Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na Corona nchini Italia yazidi ile ya China

Serikali ya Italia ilitangaza jana usiku kwamba idadi ya watu walioaga dunia kutokana na ugonjwa wa COVID-19 (corona) nchini humo imefikia 3,405.

Taarifa iliyotolewa na serikali ya Italia imesema kuwa kesi nyingine mpya za maambukizi ya watu 5322 pia zilisajiliwa katika masaa 24 yaliyopita nchini humo na kuongeza kuwa, hadi kufikia jana jioni watu 41,035 walikuwa wameambukizwa virusi vya corona.

Takwimu hizo za kufariki dunia watu 3,405 nchini Italia kutokana na virusi vya corona zinaonyesha kuwa idadi ya watu waliouawa na virusi hivyo nchini humo sasa imepita ile ya waliouawa na virusi hivyo nchini China ambao walikuwa watu 3,245.

Kutokana na kasi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona, Jumanne iliyopita Waziri Mkuu wa Italia, Giuseppe Conte alitangaza karantini katika maeneo yote ya nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 60.

Jumatano iliyopita peke yake, watu 475 waliaga dunia nchini Italia kutokana na virusi vya corona na idadi hiyo ndiyo ya juu na kubwa zaidi ya wahanga wa virusi hivyo kutokea siku moja katika upeo wa dunia nzima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *