Harriet Nyaiko alijikuta chumba cha maiti akidhaniwa amekufa

Harriet Nyaiko alijikuta chumba cha maiti akidhaniwa amekufa

Harriet Nyakio
‘Niliwekwa chumba cha maiti kwa kudhaniwa kuwa mfu’

Alipokuwa na miaka 21, Harriet Nyakio anakumbuka usiku mmoja majira ya saa tisa usiku wa manane alipohisi baridi kali isiyo ya kawaida.

Alipojipapasa aligundua kuwa hakuwa na mavazi. Wasiwasi ulimjaa akilini akijaribu kubaini ni nini kilichokuwa kimetendeka. Je, alikuwa anaota tu au ulikuwa uhalisia?

Alichokuwa bado hajafahamu ni kwamba alikuwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti, akisubiri kufanyiwa uhifadhi wa maiti.

Alikuwa amehamishiwa huko baada yake kuzimia na kutoonesha dalili za uhai kwa karibu siku nzima.

Madaktari na wahudumu waliokuwa wameuleta mwili mwingine wa mngonjwa aliyekuwa amefariki baada ya kuugua ndio waliomsikia Harriet Nyakio akiwa anajaribu kupumua na kuamka kutoka kwenye ‘usingizi wa kifo’.

“Wale wahudumu walinikuta jinsi nilivyokuwa nimehifadhiwa, waliniondoa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti , hadi kwenye wadi,” anasema.

“Daktari aliyekuwa kwenye zamu aliniuliza jina langu, nami sikusita. Nilimfahamisha mimi ni nani na maelezo kuhusu maisha yangu,” Harriet anakumbuka.

Aligundua baadaye kwamba hospitali hiyo ilikuwa ile ile ambayo alikuwa akifika kupokea dawa za kila mwezi za ugonjwa wa kifafa.

Wahudumu wa Harriet walipata nambari ya simu ya mama yake kutoka kwenye rekodi zao na kumpigia mama yake.

Baada ya kukaa siku kadhaa hospitalini aliruhusiwa kuondoka.

Unyama kabla ya kuokolewa

Harriet Nyakio, ambaye sasa ana miaka 27, anasema alikuwa na uhusiano wenye misukosuko na mama yake mzazi.

Tangu alipoanza kubaleghe anasema hawakuwa wanapatana katika mambo mengi.

Na akiwa na miaka 21 alitoroka nyumbani na kuanza kulala mitaani.

Mchana alikuwa anafanya vibarua vya hapa na pale, kisha jioni alikuwa anatafuta sehemu iliyokuwa salama na kulala.

“Basi kama kawaida usiku mmoja nilielekea sehemu niliyokuwa nalala, na haikunichukua muda mrefu kwa usingizi kunichukua,” anasema.

Alizinduliwa na kelele na fujo kutoka kuwa genge la wanaume watano waliomvamia ghafla.

“Mmoja baada ya mwingine walianza kunibaka, alipofika mtu wa tatu nilipoteza fahamu,” anasema.

Bila kujua, alikuwa ameshikwa na ugonjwa wa kifafa kutokana na mshtuko alioupata.

“Kulingana na nilivyoelezwa baadaye, wale wanaume walipomaliza shughuli yao, walinibeba hadi kwenye reli. Waliniweka katikati kwa kusudi kuwa gari moshi likipita saa za machweo liniue ,” Harriet anasema.

Lakini mambo hayakwenda hivyo.

Mwendo wa saa kumi na moja alfajiri , alichukuliwa na msamaria mwema aliyekuwa anaenda zake na kumuweka kando ya reli, chini ya mti.

Polisi walipoelezwa kuhusu mwili wa mwanamke kuonekana sehemu hiyo, walivyomkuta akiwa amezingirwa na nzi na kufunika macho yake hawakudhani angekuwa hai.

Polisi walimpeleka hadi chumba cha kuhifadhia maiti na kumuacha huko wasijue kuwa alikuwa hai ila alipoteza fahamu aliposhikwa na kifafa.

Harriet Nyakio
Maelezo ya picha,Harriet alikuwa na ugonjwa wa kifafa

Alipataje ugonjwa wa kifafa?

Harriet Nyakio alizaliwa katika kaunti ya Kerogoya, eneo la mlima Kenya.

Alizaliwa wakati mama yake alipokuwa kidato cha pili shule ya sekondari.

Baada ya mwezi mmoja mama yake alirejea kusoma na akiachwa chini ya malezi ya bibi na babu.

Kwa hivyo, Harriet alikuwa akiwafahamu bibi na babu kuwa walezi wenye kushughulikia mahitaji yake yote. Alipohitimu miaka minne alianza shule kijijini kwao.

Shule aliyokuwa anasomea ilikuwa mbali kidogo na nyumbani kwao na ilimbidi atembee mwendo mrefu kiasi kwenda na kurudi kutoka shuleni.

Siku moja alipokuwa anarejea nyumbani kutoka shuleni akiandamana na watoto wengine, gari lilipoteza mwelekeo na kuwagonga.

Yeye pekee ndiye aliyeumia, na alipata majeraha mabaya

“Nilikaa chumba cha wagonjwa mahututi kwa siku 96. Baada ya kutoka hospitalini nilianza kuanguka ghafla na kupoteza fahamu. Vipimo zaidi vilipofanywa nilielezwa nilikuwa na Kifafa,” Harriet anakumbuka.

Kukataliwa shuleni

Maisha yalibadilika mno kwake kwani hata katika shule aliyokuwa anasomea wakati huo walikataa aendeleze masomo yake . Walimu walikuwa na wasiwasi kuwa ugonjwa wake Harriet ulikuwa unawaogofya wanafunzi wengine.

Shule baada ya shule akiingia tu na kushikwa na kifafa alikuwa anafukuzwa wasitake arejee tena.

Vile vile uhusiano wake na mama yake ulizidi kuathirika.

Ingawa wakati mmoja mamake alimchukua kuishi naye mjini, kulingana na Harriet haikuwa rahisi.

Kuanzia ilipogunduliwa ana ugonjwa wa kifafa hadi leo Harriet amekuwa akitumia dawa za kumeza kila siku kuzuia hali hiyo.

Kubakwa tena

Harriet Nyakio
Maelezo ya picha,Harriet Nyakio alikataliwa shuleni

Kila wakati Harriet alikuwa anajiuliza maswali mengi kimoyomoyo kuhusu hali yake.

“Iweje nipelekwe kwenye chumba cha kuhifadhi maiti? Je mbona hawakunipima kubainisha nimekata roho? “

Lakini hakuwa na wa kumjibu aliporejea hospitalini baada ya tukio hilo.

Baada ya kupata nafuu, alirejea nyumbani kwao lakini haikuchukua muda kutoroka tena kwani bado uhusiano wake na mama ulikuwa wa changamoto sana.

Alianza kuishi mitaani tena japo kwa uoga mno.

“Nyakati za usiku sikuwa ninalala vyema , nilikuwa na wasiwasi wa kubakwa. Nilikuwa sana ninalala nikiwa nimeketi. Japo tulikuwa tunalala tukiwa vikundi vya watu wasiokuwa na makazi, mimi sikuwa na imani na mtu yeyote,” Harriet anasema.

Kisa cha pili cha chake kubakwa hata hivyo hakikutokea akiwa amelala.

Ilikuwa ni wakati akitembea kutoka shughuli zake za siku. Alikumbana na wanaume ambao anadhania in wale wale waliombaka mara ya kwanza.

Walimtendea unyama na kumtupa kwenye ua wa miiba, miiba iliyomchoma mwili wote.

Ni wasamaria wema waliomuokoa na kumupeleka hospitalini kwa matibabu .

Harriet anasema kuwa amekumbwa na changamoto za kuripoti visa vyake kwa chifu wa eneo anakoishi.

Licha ya kuwatambua waliombaka anapuuzwa na kuitwa mtu asiye na akili timamu .

“Huwa ninakutana na baadhi ya wanaume walionitendea maovu haya. Wakati mwingine wananisalimia na ninaitikia na kwenda zangu,” Harriet anasema

Kupata upendo katika ndoa na usaidizi.

“Nilikutana na mume katika pilika pilika za kutafuta sehemu salama ya kulala, tulifahamiana kwa muda,” anasema.

“Baada ya kumueleza masaibu yangu yote , na haya kuhusu ugonjwa wa kifafa amenikubali nilivyo. Tumefunga ndoa sasa na tumebarikiwa watoto wawili.”

Mume wa Harriet hamruhusu akaribie jikoni kuwa hivyo shughuli zote za mapishi hufanywa na mumewe.

Mume wake huhakikisha kuwa kila alipo yuko salama, hususan kuepukana na hatari zinazozunguka ugonjwa wa kifafa.

Vile vile shirika mmoja linalohusika na masuala ya watu wanaougua Kifafa kwa jina Kiserem epilepsy foundation linafanya kazi kwa karibu mno na Harriet katika juhudi zake za kufanikisha kipaji alichonacho cha ushonaji wa nguo.

Ugonjwa wa kifafa husababishwa na nini?

Huu ni ugonjwa unaosababishwa na seli zilizopo katika mishipa ya fahamu, zinazopatikana kwenye ubongo wakati zinapoanza kutoa umeme (impulses) mwingi kuliko kawaida kwenda kwenye misuli na sehemu nyingine za mwili.

Hili husababisha mtu kuwa na dalili kama kuishiwa na nguvu, kichwa kuuma , kuchanganyikiwa, mwili kukakamaa, na hata kupoteza fahamu.

Hali hiyo hijirudiarudia mara kwa mara.

Chanzo kikuu kwa watu wengi hakifahamiki ila wataalamu wanasema hizi ni baadhi ya sababu:

Kurithi: Familia nyingine huwa na tatizo hili, hivyo watoto na wajukuu huzaliwa na tatizo hili.

Kuumia kichwa: Ajali zinazosababisha kuumia kwa kichwa hususan mtu anapoumia mishipa ya fahamu na mtu kuumia anaweza kupatwa na kifafa.

Uvimbe kwenye uti wa mgongo: Matatizo kwenye ubongo yanayosababishwa na matatizo kama vile saratani.

Kiharusi: Hali hiyo husababisha mtu kupooza nusu wa mwili wake na huenda ukasababisha kifafa .

Matatizo wakati mtoto anapozaliwa: Wakati mwengine mtoto hushindwa kutoka kwa njia ya kawaida na kichwa chake kubanwa sana na kusababisha kifafa. Wakati mwingine, mtoto akiwa ndani ya tumbo la mama huenda mishipa na ubongo kichwani ikakosa kuungana vyema na wakati mwingine hilo linaweza kusababisha kifafa.

Ugonjwa wa kifafa hauna tiba kamili, yaani hauponi kwa asilimia mia moja. Ukishafahamishwa una kifafa utapewa utaratibu wa matibabu yaani kumeza dawa siku zote za maisha yako , na pia kufuata baadhi ya masharti. Kwa kufuata hayo, mtu anaweza kuishi maisha ya kawaida

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *