Halmashauri ya mji wa Kahama imetoa ruzuku ya pembejeo zenye thamani ya Shilingi Milioni 17.9 kwa wakulima wenye uwezo wa kulima zaidi ya Hekari 5.

Jumla ya wakulima 39  wenye uwezo wa kulima zaidi ya hekari tano kutoka kata 10 za halmashauri ya mji wa Kahama  mkoani Shinyanga wamenufaika na ruzuku ya pembejeo za kilimo zenye thamani ya shilingi milion 17.9  katika msumu huu wa kilimo.

Hii ni Mara ya pili kwa  halmashauri hiyo kuwawezesha wakulima ambapo mwaka 2018, Jumla ya wakulima 28 walipata msaada huo wenye thamani  ya zaidi ya shilingi milioni 14 Kati ya milioni 55 zilizotengwa mwaka huo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi pembejeo hizo, mkuu wa wilaya ya Kahama, ANAMRINGI MACHA amesema mpango wa serikali kupitia halmashauri ni kuhakikisha wakulima hasa vijana wananufaika na kilimo badala ya kusubiri kutegemea ajira pekee.

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji wa Kahama, CLEMENCE MKUSA amesema  fedha hizo zinatokana na mapato ya ndani ya  halmashauri hiyo  na kwamba wataendelea kutenga  bajeti kwaajili ya kuwasaidia wakulima.

Afisa kilimo wa halmashauri hiyo, SAMSON  SUMUN  amesema msaada huo wa pembejeo unatolewa bure kwa wakulima na kwamba wanapaswa kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.

Baadhi ya wakulima waliopata pembejeo hizo wamepongeza serikali kwa kuwapa msaada huo na kuomba pembejeo hizo ziwe zinatolewa mapema ili kujiandaa kikamilifu na msimu wa kilimo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *