‘Gesti 16 zafungwa na kutozwa faini

Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, imezifungia nyumba za kulala wageni 16 zilizopo eneo la Msamvu mkoani Morogoro na kuzipiga faini ya Sh milioni moja kila moja kwa kosa la wamiliki wake kukwepa kulipa kodi.‬

Akizungumza mkoani humo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Sheila Lukuba amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya zoezi la ukaguzi wa nyumba za kulala wageni lililoanza wiki tatu zilizopita ambapo walikuwa wakipita katika nyumba hizo asubuhi na walibaini makosa mengi ikiwemo ukwepaji wa kulipa kodi.

“Zoezi hili tulilianza wiki tatu zilizopita, tulikuwa tunapita kufanya ukaguzi asubuhi lakini kulionekana na udanganyifu mkubwa sana, ‘guest house’ tulizozikuta na makosa tulizipiga faini ya Sh laki mbili kila moja, sasa leo (jana) tumerudi kuja kujiridhisha kama wamefanya marekebisho,” amesema.

“Lakini bado kwa usiku huu tumetembelea zingine 20 na 16 kati ya hizo zote tumekuta zina shida na tumezifunga na kuzipiga faini ya Sh milioni moja, nne tu ndizo tulizokuta ziko vizuri,” alieleza.

Aliendelea kwa kusema, “Mimi niwaase Wanamorogoro tutii sheria bila shuruti tulipe kwa kodi kwa manufaa ya manispaa yetu, tuna miradi mbalimbali ambayo inategemea kodi hii, udanganyifu huu hautakiwi na pia hii ni mara ya mwisho kupita na kupiga faini tukipita tena kinachofuata ni kupelekana mahakamani,”..

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *