Erdogan aapa kumpa somo mbabe wa kivita wa Libya, Khalifa Haftar

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ametishia kumchukulia hatua za kijeshi mbabe wa kivita nchini Libya, Khalifa Haftar, ikiwa ataendelea kuishambulia serikali ya mjini Tripoli inayotambuliwa kimataifa.

Haya yanajiri baada ya Haftar kuondoka katika mkutano wa upatanishi mjini Moscow bila kusaini makubalino ya kusitisha mapigano, ambayo kiongozi wa serikali ya mjini Tripoli ameyaridhia.

Akizungumza na wabunge wa chama chake mapema, Erdogan ametishia kumpa funzo Haftar.

Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Deutsche Welle, Rais Erdogan amesema atashiriki katika mkutano mwingine kuhusu amani nchini Libya, ambao utafanyika Jumapili ijayo mjini Berlin, Ujerumani, ukizishirikisha pia Ufaransa, Uingereza na Italia, na mataifa ya kiarabu kama Misri, Algeria na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Uturuki imepeleka vikosi nchini Libya kuiimarisha serikali ya Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj, na Rais Erdogan amesema vitabaki huko hadi pale utulivu utakapopatikana nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *