DRC: Majeshi yafanikiwa kuteka ngome ya waasi wa ADF

Majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanasema kuwa yamefanikiwa kuteka ngome ya waasi mashariki mwa nchi hiyo ambako mashambulio kadhaa yamekuwa yakipangwa.

Kambi ya Madina, inapatikana katika eneo lenye misitu na imekuwa ikitumiwa kwa zaidi ya miongo miwili na waasi wa Allied Democratic Forces (ADF).

Kutekwa kwake kwa kambi hiyo ni pigo kubwa kwa waasi wa ADF lakini hatua hiyo pia imekuja na gharama kubwa ya kijeshi.

Zaidi ya wanajeshi 30 waliuawa na wengine 70 kujeruhiwa vibaya wakati majeshi ya serikali yalipokabiliana vikali na waasi wa kundi la ADF karibu na mji wa Beni katika eneo linalokumbwa na ukosefu wa usalama la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Msemaji wa jeshi la serikali Meja Mark Hazukai aliimbia BBC kwamba vikosi vya usalama viliwauawa takribani waasi 40 na kutwaa ngome ya wanamgambo hao iliyoko Medina kwenye makabiliano hayo makali yaliyotokea mwishoni mwa wiki jana kwenye mkoa wa Kivu kaskazini.

Msemaji huyo alisema, kuchukuliwa kwa ngome ya Medina, ambayo ndiyo kitovu cha operesheni za waasi, ni hatua muhimu katika harakati za jeshi la taifa kutokomeza makundi ya wanamgambo hasa lile la ADF kutoka Uganda.

Eneo la Kivu kaskazini linapatikana kwenye mpaka na Uganda.

Waasi wa ADF, ambao wanatoka Uganda, wamekuwa wakiendeleza mashambulizi ya umwagaji damu mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na wamelaumiwa kwa mauaji na mateso ya raia.

Vita dhidi ya ADF na wanamgambo wengine.

Serikali ya rais Felix Tshishekedi ilitangaza kuanzishwa kwa operesheni mahususi ya kijeshi ya kutokomeza makundi ya waasi mwezi Oktoba mwaka jana, likiwemo lile la ADF, ambalo yameendeleza hujuma dhidi ya raia na kufanya eneo la mashariki mwa DRC kukosa usalama.

Kwa mujibu wa Umoja wa Matiafa, wapiganaji wa ADF wanashtumiwa kwa maaujai ya zaidi ya watu elfu moja katika eneo la Beni, kwenye mkoa wa Kivu kaskazini tangu mwaka wa 2014.

Kati ya mwezi Novemba na Desemba mwaka jana, waasi wa ADF waliwauwa raia 150.

Mauaji hayo ya waasi wamesababisha hasira miongoni mwa wakaazi wa eneo la mashariki mwa DRC, ambalo walifanya maandamano makubwa ya kupinga vikosi vya Umoja wa mataifa vinavyohudumu katika eneo hilo MONUSCO.

Raia wanalalamikia vikosi vya MONUSCO kutowalinda dhidi ya mashambulizi ya waasi.

Hali hii imesababisha majeshi ya Umoja wa mataifa kushirikiana na vikosi vya serikali katika kukabiliana na makundi ya waasi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *