DAS SIMANJIRO: ZAWADI YA MTOTO NI ELIMU.

JAMII imetakiwa kutambua kuwa zawadi kubwa wanayotakiwa kutoa kwa watoto wao ni kuwapa elimu kwani itawanufaisha kwenye maisha yao ya baadaye.
Katibu Tawala wa wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Zuwena Omary ameyasema hayo kwenye mahafali ya tisa ya shule ya awali na msingi New Light iliyopo Mji mdogo wa Mirerani.
Omary amewataka wazazi na walezi wasiwape watoto wao zawadi ambayo kesho yake hataifurahia na kuijutia hivyo urithi mzuri ni kuwapatia elimu.
Amesema unaweza kumpa mtoto wako zawadi kubwa na ya thamani lakini baadaye akaipoteza ila akiwa na elimu ni urithi wa maisha yake yote.
Mkurugenzi wa shule ya awali na msingi New Light, Askofu Sommy Severua amesema kupitia elimu mtoto wa kibarua anaweza kupata madaraka makubwa.
Askofu Sommy amesema mtoto wa mchimbaji mdogo wa madini miaka ijayo ataweza kuwa Rais wa nchi miaka ijayo endapo atapata elimu.
Amewataka wahitimu wa darasa la saba wa shule hilo kutumia elimu waliyoipata kwa mustakabali wa maisha yao ya baadaye.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo kupata wa Mirerani Adam Kobelo amesema hayo ni mahafali ya sita shule hiyo.
Kobelo amesema wanafunzi wengi waliohitimu shule hiyo wamepata mafanikio kitaaluma kutokana na msingi mzuri walioupata hapo.
Mmoja kati ya wahitimu wa mahafali hayo Gift Lyimo amesema anafuraha kubwa kumaliza elimu ya msingi na sasa anasubiria matokeo ya darasa la saba baada ya kufanya mtihani.
Lyimo amesema ana matumaini makubwa ya kufaulu kwani alipata msingi mzuri kwenye shule hiyo tangu elimu ya awali hadi darasa la saba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *