CCM yawatoa hofu wakulima wa Mbaazi Manyara.

Na Mwandishi wetu, Manyara
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kheri James ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM amewataka wakulima wa mbaazi Mkoani Manyara kuondoa hofu ya bei ndogo ya zao hilo kwani Serikali ya awamu ya tano ipo mbioni kurekebisha hilo.
James aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni ya CCM uliofanyika mtaa wa Nakwa kata ya Bagara mjini Babati.
Alisema wanatambua mbaazi ndiyo dhahabu ya wakulima wa eneo hilo hivyo watahakikisha serikali inafanikisha kwa kuweka mazingira rafiki ya bei nzuri ya zao hilo.
“Tutahakikisha soko zuri la mbaazi linapatikana hadi nje ya nchi kwa ajili ya manufaa ya wakulima wetu ili waweze kupiga hatua ya kimaendeleo katika maisha yao,” alisema.
Alisema wananchi wa eneo hilo wanapaswa kuwachagua wagombea wa CCM ili washirikiane kufanikisha maendeleo yao kuliko kuchagua wagombea wa upinzani.
Mbunge mteule wa jimbo la Babati mjini Pauline Gekul alisema wananchi wa eneo hilo wanapaswa kumchagua tena Rais John Magufuli kwani amefanikisha maendeleo mengi hapa nchini.
Gekul alisema ni maendeleo mengi yamefanyika kwenye kipindi cha utawala wa Rais Magufuli hivyo wampigie kura mgombea udiwani wa kata hiyo ili wafanikishe maendeleo mengine zaidi.
Asia alisema sumu haionjwi hivyo wananchi wa eneo hilo wajitafakari kwa kuchagua maendeleo na siyo maneno matupu yanayotolewa na vyama vingine.
Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Manyara, Mosses Komba alisema wapinzani hawana sera hivyo wananchi wachague viongozi bora kupitia CCM.
Mgombea udiwani wa kata ya Bagara mwalimu Yonah Gang’aida alisema wananchi wa eneo hilo wamchague ili ashirikiane nao kwani wanafahamu utendaji kazi wake tangu akifundisha.
“Nimewafundisha wanafunzi wengi na mnaujulia utendaji kazi wangu hivyo naombeni kura zenu tushirikiane kuijenga kata yetu, alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *