Biteko Apokea Ripoti Maalum Madini Ya Ujenzi, Viwandani

Waziri wa Madini Doto Biteko amepokea Ripoti Maalum kutoka kwa Kamati Tendaji ya Madini ya Ujenzi na Madini ya Viwandani kuhusu Changamoto zilizopo katika uchimbaji wa Madini na Masoko ya kuuzia madini hayo.

Kikao hicho kilichoongozwa na Waziri Biteko kilifanyika Desemba 16, 2019 katika Ukumbi wa Wizara ya Madini Jijini Dodoma kikiwa ni mwendelezo wa vikao vya kamati hiyo vilivyoanza Novemba 14, 2019, vikilenga kujadili changamoto wanazozipitia wachimbaji katika shughuli za uzalishaji wa madini hayo.

Waziri Biteko aliwataka viongozi wa kamati ya madini ya ujenzi na kamati ya madini ya viwandani kufanya kazi kwa ushirikiano ili waweze kufanikiwa na kuwaahidi kuzifanyia kazi changamoto zao.

“FEMATA wamefanikiwa katika shughuli zao si kwa sababu wana akili sana ila wanashirikiana kwenye maamuzi yao, na mimi pia nashirikiana kwa karibu sana na Rais wenu wa FEMATA John Bina, migawanyiko itawafanya msifanikiwe”, alisema Biteko.

Aidha, Waziri Biteko amempongeza Rais wa Wachimbaji Wadogo John Bina kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuliongoza Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA) na kuwataka wachimbaji wa madini kote nchini kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na serikali katika Sekta ya Madini.

“Kazi ya kusimamia rasilimali ya madini sio ya wizara peke yake ila ni kazi ya wananchi wote wakiwemo FEMATA, wachimbaji wenyewe na wadau wote wa madini,”alisisitiza Biteko.

Aliongeza kuwa, Serikali inawathamini wachimbaji na wanachopaswa kuelewa ni kwamba sekta inazo changamoto nyingi na haziwezi kuisha kwa siku moja na kusema, “mimi binafsi ukiniuliza ninatamani nione wachimbaji wanafurahi, nione watu wote kwenye sekta wanafurahi,” Biteko alisema.

Pia, Waziri Biteko amesema ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) inaonesha usafirishaji wa Madini nje ya nchi umepanda kwa asilimia 48 kutoka mwezi Oktoba 2018 hadi Oktoba 2019, na kusema kwamba, hiyo inaonesha wachimbaji wamekubali kufuata Sheria.

Wakati huo huo, Waziri Biteko aliwataka Watendaji wa Tume ya Madini wanaohusika na masuala ya utoaji Leseni kutochelewesha leseni hizo pindi waombaji wanapoomba.

Kwa upande wake, Rais wa Wachimbaji Wadogo John Bina alimuomba Waziri Biteko kuzifanyia kazi changamoto zilizopo kwenye taarifa hiyo ikiwemo suala la utoaji wa vibali vya kusafirisha Madini nje ya nchi kwani imekuwa changamoto katika shughuli zao.

“Tunakushukuru sana Waziri kwa kutukutanisha na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, pia sisi kama shirikisho la wachimbaji tunaamini kwamba ili tumalize matatizo yetu na serikali lazima tukae meza moja tuzungumze, hatupendi FEMATA ikawa ni chama cha harakati, tunapenda kiwe chama cha kazi na mashauriano,” Rais Bina alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *