Baraza la mji wa Minneapolis laahidi kuvunja idara ya polisi

Idadi kubwa ya maafisa wa baraza la mji wa Minneapolis wameahidi kuivunjilia mbali idara ya jeshi la polisi, hatua muhimu huku kukiwa na maandamano ya kitaifa yaliosababishwa na kifo cha George Floyd mwezi uliopita.

Madiwani tisa kati ya 13 walisema kwamba mfumo mpya wa kuweka usalama wa umma utabuniwa katika mji ambao wasimamizi wa usalama wameshutumiwa kwa ubaguzi.

Meya Jacob frey mapema alipinga hatua hiyo na kuzomwa na wakaazi.

Maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi yameandaliwa baada ya kifo cha Floyd katika mikono mwa polisi.

Hatahivyo mikakati ya kiusalama kote nchini humo iliondolewa siku ya Jumapili huku hali ya wasiwasi ikiendelea kupungua.

Mazishi ya Floyd yanapangwa kufanyika siku ya Jumanne mjini Houston ,ambao ndio mji anaotoka kabla ya kuhamia Minneapolis.

Maandamano hayo yalianza baada ya kanda ya video kuonekana ikimuonyesha amelazwa barabarani, huku afisa wa polisi mzungu akiwa amemuwekea goti shingoni kwa takriban dakika tisa.

Afisa wa polisi Derek Chauvin amefutwa kazi na kushtakiwa kwa kutekeleza mauaji.

Maafisa wengine watatu ambao walikuwa katika eneo hilo pia wamefutwa kazi na kushtakiwa kwa kuruhusu na kuendeleza kilichotokea.

Je baraza la mji wa Minneapolis linasema nini?
Madiwani tisa walisoma taarifa kwa mamia ya waandamanaji siku ya Jumapili.

”Tuko hapa kwasababu hapa Minneapolis na miji mingine kote Marekani ni wazi kwamba mfumo uliopo wa usalama haulindi jamii”, alisema rais wa baraza hilo Lisa Bender ambaye alinukuliwa akisema.

”Juhudi zetu za kufanya mabadiliko zimefeli. moja kwa moja”.

Bi Bender alisema kwamba maelezo kuhusu uvunjaji huo yanahitajika kujadiliwa zaidi, akiongezea kwamba atajaribu kuhamisha ufadhili wa polisi kwa mikakati inayowekwa na jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *