Aussems: Hakuna wa kuzuia ubingwa Simba

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems, amefunguka kuwa ana uhakika mkubwa wa timu yake kuweza kutetea ubingwa wake msimu huu licha ya kupoteza mchezo uliopita kutokana na ubora wa kikosi chao.

Simba bado inaongoza ligi ikiwa na pointi 18 kabla ya mchezo wa jana Jumapili dhidi ya Mbeya City na nyuma ya Kagera Sugar wenyewe pointi 16, wakati wapinzani wao wakubwa Azam wakiwa kwenye nafasi ya 13 wakiwa na pointi tisa huku Yanga wakiwa na pointi saba kwenye nafasi ya 17.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Aussems amefunguka kuwa bado wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa msimu huu na hakuna ambacho kitaweza kuwazuia kutokana na kasi ya wapinzani wao huku akiamini ubora wa timu yake kubadilika baada ya kufungwa na Mwadui wiki iliyopita.

“Haikuwa mipango yetu kupoteza lakini wachezaji na benchi la ufundi tumegundua makosa yetu ambayo yamesababisha kutuondoa kwenye njia ingawa haijaweza kuharibu malengo ambayo tupo nayo kwenye ligi, maana ukiangalia wapinzani wetu wakubwa bado hawapo sawa.

“Sisi kwa sasa tunaangalia nini ambacho tunahitaji kufanya ndani ya ligi kwa kuwa hesabu zetu ni kutetea ubingwa na hatuoni am­bacho kinaweza kutuzuia kwa sasa kutokana na ubora wa timu yetu, kila mchezaji anatambua na kuelewa nini ambacho tuna­paswa kukipigania kuhakikisha tunatimiza malengo ambayo tu­mejiwekea,” alisema Aussems.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *