Aliekutwa na nyama ya twiga atakiwa kulipa Milioni 333

Mshtakiwa katika shauri namba 11/2018 ya uhujumu uchumi na makosa ya kupanga Omari Bokoi amehukumiwa kulipa faini ya Milioni 333 au kwenda jela miaka 20 baada ya Mahakama ya Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro kumkuta na hatia ya kupatikana na vipande vya nyama ya Twiga .

Hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Same Helen Hoza pia iliwaachia huru washtakiwa wengine wawili katika shauri hilo, mshtakiwa wa pili Omari Mnoa na wa tatu Peter Charles baada ya kukosekana kwa ushahidi wa kutosheleza kuwatia hatiani.

Bokoi amehukumiwa baada ya kupatikana nyara za serikali kinyume cha sheria ya uhifadhi wa wanyama pori namba 5 ya mwaka 2009 inayosomwa sambamba na kifungu cha 14 cha jedwali namba 1 na kifungu namba 57 kifungu kidogo cha kwanza na kifunga cha 60 kifungu kidogo cha pili cha sheria ya uhujumu uchumi na makosa ya kupanga.

Akisoma maelezo ya kosa kwa watuhumiwa hao Hakimu Hoza alieleza kuwa mnamo October 15 mwaka 2018 katika eneo la Muheza jirani na Hifadhi ya taifa ya Mkomazo wilayani Same washtakiwa hao walikutwa na vipande vya nyama ya Twiga .

Alieleza kuwa mshtakiwa alikutwa na gunia moja likiwa na vipande hivyo ambavyo vinatajwa kuwa sawa na mnyama mmoja aliyekuwa ameuawa ,akiwa na amebeba kwenye pikipiki yake aina ya Boxer ikiwa na namba za usajili Mc 661 ATV.

Hoza alieleza kuwa thamani ya nyama aliyokutwa nao mshtakiwa inafikia kiasi cha Milioni 33,300,000 sawa na Dola za marekani 15000 na kwamba mshitakiwa hakuwa na kibali cha umiliki kutoka kwa mkurugenzi wa wanayama pori nchini .

Katika shauri hilo Mwendesha mashtaka wa shirika la Hifadhi za taifa (TANAPA) Samuel Magoka kwa niaba ya Jamhuri aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa yeyote mwenye nia ya kufanya vitendo vya ujangili kwa nyara za taifa.

Aliieleza Mahakama kuwa wanyama jamii ya Twiga wameendelea kutoweka na serikali iimekuwa ikitumia gharama kubwa katika kuwalinda ,pia ni nembo ya taifa na ni kivutio cha watalii katika kuiingizia serikali fedha za kigeni.

Akiwasilisha maombolezo mshitakiwa Bokoi aliiomba mahakama kumuonea huruma kwa kuwa ana mke na mtoto mmoja ambao wanamtegemea na kwamba amekaa rumande kwa muda wa miaka miwli kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Hoza akasoma hukumu iliyomtia hatiani baada ya kuridhika na ushahidi kutoka kwa mashaidi sita pamoja na vielelezo tisa vilivyowasilishwa mahakamani hapo.

Mshtakiwa baada ya hukumu kutolewa ameshindwa kulipa faini hivyo ataenda kutumikia miaka 20 jela.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *